Mabaki ya mwili wa Naomi aliyeuawa na mumewe, kuzikwa upya
Baba mdogo wa marehemu Naomi Marijani, Robert Marijani amesema kuwa kama familia watazika upya mabaki ya mwili wa Naomi, baada ya kesi kumalizika.
Marijani ameyasema hayo leo Februari 26,2024 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kumuhukumu mfanyabiashara, Khamis Luwongo, kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mke wake Naomi Marijani na kisha mwili wake kuuchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa na lita tano za mafuta ya taa, na kuchukua majivu pamoja na mabaki ya mifupa yake na kwenda kuyazika katika shamba lake lililopo kijiji cha Marogoro, Wilaya ya Mkuranga.