Marekani imeiunga mkono na kuegemea upande wa Russia katika upigaji wa kura mbili za Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo wa Russia dhidi ya Ukraine.
Nchi hizo mbili zilipinga azimio lililoungwa mkono na Ulaya katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) siku ya Jumatatu, ambalo lilikemea vita ya Russia dhidi ya Ukraine.
Baadaye, katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), wote walipitisha azimio lililoungwa mkono na Marekani likitaka kumalizika haraka kwa mzozo huo, bila kuitaja Russia kama mvamizi ama kuitetea Ukraine iwapo inapaswa kurejeshewa maeneo yake.
Uingereza na Ufaransa, ambazo zina viti vya kudumu katika baraza hilo pamoja na Marekani, Russia na China, zilijizuia kupiga kura kuhusu azimio la pili la mkutano huo.
Wanachama wa muda wa baraza hilo Denmark, Ugiriki, na Slovenia pia hawakupiga kura kuhusiana na suala hilo.
Kura hizo, zilizopigwa wakati wa kumbukumbu ya miaka mitatu tangu Russia itangaze kuanza Operesheni yake ya kijeshi nchini Ukraine.
Kupigwa kwa kura hizo kunaonyesha tena mgawanyiko mkubwa kati ya washirika wa Magharibi, huku Rais, Donald Trump akibadilisha msimamo wa Marekani kuhusu kuisaidia Ukraine, ishara ya kuachana na sera ya mambo ya nje ya muda mrefu katika taifa hilo.
Utawala wa Trump umeitekeleza Ukraine tofauti na ilivyokwa kwenye utawala wa Rais Joe Biden ambaye alimkumbatia Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy huku akimpelekea kila misaada ya kijeshi aliyohutaji kutoka Marekani.
Mambo yalianza kwenda kombo kwa Zelensky baada ya Rais Trump kutangaza kuanza maandalizi ya kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Rais wa Russia, Vladimir Putin huku akimpigia na kuongea kwa takriban dakika 90 jambo lililomkera Zelenskyy.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.