Kundi la kwanza la askari wa Jeshi la Ulinzi la Afrika Kusini (SANDF) waliojeruhiwa katika mapigano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) limeanza kurejea nyumbani kupitia Kigali, nchini Rwanda baada ya kukwama katika kambi zao kwa karibu mwezi mmoja.
Wanajeshi hao ni miongoni mwa askari wa SANDF walioko chini ya Kikosi cha Walinda Amani wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SAMIDRC), wanaoimarisha ulinzi Mashariki mwa DRC sambamba na kukabiliana na uovu wa waasi wa M23 dhidi ya raia.
Televisheni ya Afrika Kusini ya SABC imesema, wanajeshi hao ambao walishindwa kupambana na M23 kwa kushindwa kuwadhibiti kuitwaa Miji ya mashariki mwa nchi hiyo, walionekana wakiondoka Mjini Goma kuanzia juzi jioni kwa barabara bila vifaa na sare zao za kijeshi.
Ripoti ya jarida la Afrika Kusini la Rapport iliyochapishwa Jumapili ilieleza kuwa wanajeshi wa Afrika Kusini waliojeruhiwa ni 189.
Kwa mujibu wa jarida hilo, miongoni mwa waliojeruhuwa ni wanajeshi wawili ambao ni wajawazito, huku idadi ya wanajeshi wa SANDF wanaoendelea kukwama nchini DRC ikikadiriwa kuwa kati ya 1,000 na 2,000.
Katika video zilizopakiwa na waandishi wa habari wa eneo hilo, wanajeshi walionekana wakiondoka Mjini Goma Jimbo la Kivu Kaskazini na kuingia Rwanda wakiwa wamevalia mavazi ya kiraia.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.